Arusha:
Wakati askari polisi saba watatoa ushahidi mahakamani katika kesi ya
uchochezi inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema,
Mahakama imetoa onyo kwa askari Polisi na Magereza wanaowasumbua
waandishi wa habari na wananchi.
Onyo hilo lilitolewa na Hakimu Mkazi
Mfa- widhi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Augustino Rwezile baada ya
askari Magereza kuwafukuza kwa mbio huku wakiwa na silaha waandishi wa
habari waliotaka kuchukua kumbukumbu za Lema kufikishwa mahakamani.
Pia, aliwaonya Polisi ambao wamekuwa wakilalamikiwa kwa kuwazuia wananchi wanapokwenda kusikiliza kesi ya mbunge wao.
Waandishi wa habari jana waliwahi
asubuhi kusikiliza kesi ya Lema na kutaka kumpiga picha wakati
akifikishwa mahakamani, lakini walipata wakati mgumu baada ya kukimbizwa
na askari Magereza wenye silaha ambao hawakutaka mtu yeyote kupiga
picha ya mtuhumiwa huyo.
Waandishi hao, Lilian Joel (Uhuru) na
Janet Mushi (Mtanzania) waliokolewa na Hakimu Mkazi, Nestory Baro ambaye
walimshika huku wakipiga kelele kuomba msaada hatua ambayo ilizua
tafrani mahakamani.
Hata hivyo, baada ya tukio hilo,
waandishi hao walipelekwa na hakimu Baro kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi,
Rwezile ambaye alishuhudia pia tukio hilo.
Hakimu Rwezile aliwaita maofisa wa
Polisi, waliokuwa mahakamani hapo na kuwaonya kuacha tabia ya kuwakamata
na kuwabughudhi wananchi na wanahabari wanaofika mahakamani hapo
kusikiliza kesi.
Hakimu Rwezile, pia alilitoa agizo
hilo la kuwaonya askari Magereza na Polisi baada ya wakili wa Lema, John
Mallya kuomba tamko la mahakama kutokana na wananchi kuzuiwa kuingia
mahakamani, kukamatwa na kunyanyaswa waandishi wa habari.
Hakimu Rwezile alitoa agizo tena kwa
askari Magereza na Polisi wanaofika mahakamani kuacha kuwasumbua
wananchi na kueleza pamoja na wanahabari wana uhuru wa kufika mahakamani
na kusikiliza kesi.
“Hakuna usiri mahakamani
hatutarajii tena kuona misuguano hapa, tayari nimezungumza na waandishi
na askari Magereza kuhusiana na suala hili, eneo hili lipo chini ya
Mahakama hivyo watu wanapaswa kuingia na kutoka salama,” alisema
Jana saa mbili asubuhi, Lema
alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha kwa basi la
Magereza, akiwa chini ya ulinzi mkali na haikuruhusiwa kumpiga picha.
Mbele ya Hakimu Rwezile, wakili wa
Serikali, Fortunatus Mhalila alisoma maelezo ya awali ya kesi hiyo na
kudai upelelezi umekamilika na upande wa Jamhuri una mashahidi saba.
Aliwataja mashahidi hao kuwa ni Ofisa
Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Arusha (RCO), SSP George Katabazi, Mkuu wa
Upelelezi wa Polisi Wilaya ya Arusha (OSCID), ASP Damas Masawe, Mkaguzi
wa Polisi, Adam Nyamiti, WP 6826 Ester Yohana na Ofisa wa Kitengo cha
Upelelezi Makosa ya Mtandao Makao Makuu ya Polisi, Ezekiel Kway.
Alidai katika kesi hiyo, Lema
anatuhumiwa kuhamamisisha watu kutenda kosa ikiwa ni kinyume na kifungu
390 (35) cha Kanuni za Adhabu, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Mhalila alidai Lema kati ya Agosti
Mosi hadi 26, alitengeneza na kusambaza ujumbe mfupi wa sauti kupitia
WhatsApp kuhamasisha watu kutenda kosa, ikiwapo kuwataka kufanya
maandamano kuanzia Septemba Mosi mwaka huu. Baada ya maelezo hayo,
Hakimu Rwezile alimtaka Lema kueleza kama maelezo hayo ni sahihi au la.
Lema alikanusha kutuma ujumbe wa
kuhamamisha uvunjaji wa sheria. Wakili Mallya alisema upande wa utetezi
upo tayari kupangwa kwa siku ya kuanza kuwasikiliza mashahidi. Kutokana
na maelezo hao, Hakimu Rwezile aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 2,
ushahidi utakapoanza kutolewa.
Lema na mkewe, pia wana kesi nyingine
ya kutoa lugha ya uchochezi dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho
Gambo ambayo nayo iliahirishwa hadi Desemba 21 kutokana na mtuhumiwa wa
pili, Neema Lema (33) kutokuwapo mahakamani.
Wakili Mallya alisema Neema ameitwa
jijini Dar es Salaam katika kesi nyingine. Baada ya maelezo hayo, Hakimu
Rwezile aliahirisha kesi hiyo na Lema kurejeshwa magereza hadi leo,
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha itakapoanza kusikiliza maombi ya dhamana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni