Watu wawili wanaotuhumiwa kula nyama za
binadamu wamekamatwa baada ya kichwa cha mtoto wa miaka mitatu, kukutwa
katika nyumba wanayoishi nchini Pakistan.
Polisi waligundua tukio hilo la kutisha
na kuwakamata watuhumiwa Mohammad Arif Ali (35) na mdogo wake Mohammad
Farman Ali mwenye miaka 30.
Kwa mujibu wa gazeti la mtandaoni la
Dailymail, wanandugu hao wanaotoka katika mji mdogo wa Darya Khan
wamewahi kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, baada ya kutiwa
hatiani kwa makosa ya kula nyama za binadamu. Waliachiwa huru baada ya
kumaliza kutumikia adhabu hiyo mwaka jana.
Arif na Farman walikamatwa na kuswekwa
rumande wakati uchunguzi ukiendelea, baada ya tukio hilo lililowavuta
wengi na kutikisa tena eneo hilo.
Miaka mitatu iliyopita ndugu hao
walifukua zaidi ya miili 100 ya maiti katika makaburi yaliyopo karibu na
kijiji chao kisha kuzitumia maiti hizo kama asusa.
Mkuu wa Polisi katika eneo hilo, Ameer
Abdullah alisema maofisa wake wa polisi waliamua kuvamia na kufanya
upekuzi katika eneo hilo, baada ya majirani kulalamika kwamba kuna
harufu mbaya ambayo imekuwa ikitoka katika nyumba waliyokuwa wakiishi.
“Wakazi hao waliifahamisha polisi baada
ya kusikia harufu mbaya ikitokea katika nyumba waliyokuwa wakiishi watu
hawa,” alisema Abdullah.
Abdullah alisema: “Tulifika katika
nyumba hiyo siku ya Jumatatu asubuhi na kufanya upekuzi kabla ya kukiona
kichwa cha mtoto wa miaka mitatu.
“Baada ya kugundua kitu hicho
kinachotisha, tulimkamata mmoja wa ndugu hawa Mohammad Arif na
alitupatia ushirikiano hadi tulipomweka kizuizini ndugu yake,” alisema
Abdullah.
Alisema jeshi la polisi bado linaendelea
na uchunguzi ili kung’amua iwapo kuna makaburi mengine yamechimbwa na
watu hao kijijini hapo au katika vijiji vya jirani.
Baada ya kuulizwa maswali mengi na
polisi, ndugu hao walikiri kula nyama za watu na kueleza ukweli namna
walivyokuwa wakitengeneza mlo huo. Kwa kuwa Pakistan haina sheria
zinazohusu ukatili wa maiti, huenda haitakuwa rahisi kwa wawili hao
kufungwa jela maisha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni