Ijumaa, 21 Machi 2014

JOHN DE MKALI. IKULU YAMTAKA ASKOFU KAKOBE AACHE POROJO NA MANENO

Kurugenzi ya mawasiliano Ikulu imesema haina muda wa kujibu porojo zilizotolewa na Askofu wa kanisa la Full Gospel Fellowship, Zachary Kakobe kwani ina kazi kubwa ya kuwatumikia watanzania.


Imesisitiza kuwa ofisi ya Kurugenzi ya mawasiliano Ikulu haifanyi kazi za porojo kama sehemu ya kuendesha utawala wake, badala yake iko makini kutatua matatizo yanayowakabili wananchi kwa kulinda na kuheshimu demokrasia na kufuata katiba ya nchi.

Kauli hiyo inatokana na waraka maalumu unaodaiwa kutolewa na Askofu Kakobe na kisha kupelekwa Ikulu.Hata hivyo, kurugenzi ya mawasiliano Ikulu imesema haijathibitisha rasmi kama waraka huo umefika katika ofisi hiyo.

Akizungumza juzi na gazeti la Jambo Leo kwa njia ya simu,Mkurugenzi wa idara ya mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu alisema serikali si lazima ijibu Porojo zilizotolewa na Kakobe, kwani Ikulu ni sehemu nyeti ya kutumikia wananchi katika maswala ya msingi na yenye tija kwa taifa.

"Yaani unataka niseme mambo ya porojo badala ya kuelekeza majibu yenye kutatua matatizo ya wananchi",

alisema na kuongeza kuwa swala hilo lilishajibiwa na kaimu katibu mkuu ofisi ya waziri mkuu, Dr Florence Turuku ambapo alilitolea ufafanuzi wa kutosha.

Waraka huo uliotolewa kwenye vyombo vya habari na Askofu Kakobe ulikuwa ukieleza namna Ikulu "ilivyotupa kapuni" majina yote ya wapentekoste waliopendekezwa kuwa wajumbe wa bunge maalumu la katiba, hivyo kuwafanya wapentekoste takribani milioni 10 kukosa mwakilishi hata mmoja.

Pia waraka huo ulidai kuwa baada ya kukosa uwakilishi, Ikulu ilitoa kauli za kejeli kuwa, haijawahi kupokea jina hata moja la mpentekoste.

"Ofisi yako imeona kwamba ni haki hata kwa waganga wa kienyeji kuwakilishwa katika bunge hilo kuliko wapentekoste kupata mjumbe hata mmoja", ilisema sehemu ya waraka huo.

Hata hivyo baadhi ya wananchi waliohojiwa na gazeti la Jambo Leo walisema Askofu Kakobe amezoea kulumbana na Serikali, hivyo uamuzi wake hauna mashiko.

"Tunajua ana waumini wengi wanaomsikiliza, lakini kwa maswala ya kiserikali ambayo inaaminika haina dini ni vigumu kuitabiria mabaya, kwani yeye kama mchungaji alistahili kukaa pamoja na ofisi husika na si kwenda kunukuu vitabu vitakatifu kwa kuitabiria mabaya serikali",
Alisema Patrick Haule ambaye ni Mwinjilisti. 

Chanzo: Gazeti la Jambo leo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni