Mjumbe wa Bunge la Katiba, Almas Maige
amesema endapo wajumbe wa Bunge hilo watapitisha muundo wa Serikali
tatu, nchi itaingia katika kitabu cha maajabu ya dunia cha Guiness Book
of Records.
“Hili litakuwa shirikisho la pekee hapa
duniani lenye marais wengi katika nchi mbili, linaweza kuingia katika
kitabu cha maajabu cha Guiness kwa kuwa na marais wengi katika nchi
maskini sana,” alisema.
Mjumbe huyo alisema amejaribu kufuatilia
hoja za wanaounga mkono muundo huo na kufananisha na nchi za Marekani
na Nigeria, lakini akasema katika nchi hizo Rais wa nchi ni mmoja.
“Mimi nimejaribu kuwafuata
wanaofananisha na Marekani na Nigeria, wameshindwa kusema katika nchi
hizo mbili Rais ni mmoja tu hakuna wingi wa Rais kutokana na majimbo,”
alisisitiza.
Katika hatua nyingine, mjumbe huyo
aliwashangaa wajumbe wanaotokana na kundi la Ukawa kujigeuza kuwa
wachunguzi wa kijinai kwa kuhoji uhalali wa saini ya muasisi wa
Muungano, Abeid Aman Karume.
“Mimi nawashangaa sana wanasiasa hawa na
wanasheria wa Ukawa wamejigeuza Forensic Expert (wachunguzi wa jinai).
Mimi ningewaunga mkono kama wangeenda kuwauliza watoto wa marehemu,”
alisema.
Aliongeza kusema: “Watoto wa marehemu
wapo Zanzibar… Yupo Aman Karume aliyekuwa Rais wa Zanzibar na yuko
Balozi Ali Karume na yuko pia mama Karume. Kwa nini hawawaulizi,”
alihoji.
“Mimi ningefurahi sana kama wangeenda
kuwauliza wanafamilia sahihi hii ni ya baba yenu? Au je, mheshimiwa mama
hii ni sahihi ya mumeo? Wangekataa ndipo tungewaunga mkono,”
alisisitiza.
Mjumbe huyo alisema kinyume chake, Ukawa
wanavaa gamba la elimu ambayo hawana na vilevile hawajui maana na
tafsiri sahihi iliyoandikwa miaka 50 iliyopita.
“Taaluma ya sasa ingeweza kugundua wino
uliotumika una umri gani na kuondoa kero hiyo kama ni ya juzi au jana au
kama imeghushiwa,” alisema mjumbe huyo na kuongeza kusema:
“Wataalamu wa Forensic (uchunguzi wa
kijinai) wangeweza kugundua wino huo una miaka 50. Wanafanya kitu
ambacho hawakijui na wanadhalilisha Watanzania.”
Mjumbe huyo alisema yeye anaunga mkono muundo wa Muungano wa Serikali mbili na kuwa Serikali tatu ni sawa na mtu kunywa sumu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni