Nahodha wa kivuko cha Korea Kusini
kilichozama na kusababisha watu zaidi ya 300 kutojulikana walipo
amekamatwa Jumamosi (19.04.2014) kwa tuhuma za uzembe na kuwatelekeza
watu waliokuwa kwenye shida ya kuhitaji msaada. Wapelelezi
wamemkamata
Lee Joon -Seok na wafanyakazi wenzake wawili mapema leo asubuhi na wote
watatu wameshutumiwa kwa kuwatelekeza mamia ya abiria waliokuwa wamenasa
ndani ya chombo hicho na kuhangaika wenyewe kujiokowa. Mahakama imesema
imeamuru kukamatwa kwao ili kuzuwiya watuhumiwa hao kukimbia au
kuharibu ushahidi.
Nahodha huyo mwenye umri wa miaka 68
yuko chini ya uchunguzi kwa kuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kuitelekeza
meli hiyo wakati abiria wake wakiwa bado wako hatarini.Lee amefunguliwa
mashtaka ya uzembe na kushindwa kuhakikisha usalama wa abiria kinyume
na sheria za bahari.Abiria waliambiwa kupitia vipaza sauti kwamba
wabakie hapo walipo licha ya kuwa meli hiyo ilikuwa ikizama upande
mmoja.
Nahodha atetea uamuzi wake
Watu 32 imethibitishwa kuwa wamekufa
katika janga hilo na wengine 270 hawajulikani walipo wengi wao ni watoto
wakiwa katikasafari ya shule ya upili.
"Naomba radhi kwa wananchi wa Korea
Kusini kwa kusababisha janga hili na nainamisha chini kichwa changu
kuomba radhi familia za wahanga" Lee amewaambia waandishi wa habari
wakati akiondoka katika mahakama ya Wilaya ya Gwangiu Tawi la Mokpo
kuelekea gerezani leo asubuhi. Lakini ametetea uamuzi wake ulioshutumiwa
vikali wa kusubiri dakika 30 kabla ya kuamuru kuchukuliwa kwa hatua za
kuondolewa kwa abiria.
"Wakati huo mawimbi yalikuwa makali
sana, hali ya bahari ilikuwa ya baridi,na nilifikiri kwamba iwapo watu
wataondoka kwenye kivuko hicho bila tafakuri inayofaa na ikiwa hawakuvaa
majeketi ya uokozi na hata ingelikuwa wamevaa, wangelisombelewa mbali
na maji na kukabiliwa na matatizo mengine magumu" Lee amesema na
kuongeza kwamba meli za uokozi zilikuwa bado hazikuwasili na pia
kulikuwa hakuna meli zozote zile za uvuvi au mashua nyengine karibu
wakati huo.
Watu wengi wangeliweza kuokoka
Wataalamu wamesema watu wengi zaidi
wangeliweza kunusurika ingelikuwa wameondoka kwenda vituo vya uokozi
kabla ya meli hiyo kuegemea sana upande mmoja na maji kuanza kujaa
ndani.
Msaidizi wake wa tatu mwenye umri wa
miaka 26 ambaye alikuwa na uzoefu wa miezi sita katu hakuwahi kabla
kuongoza meli hiyo kwenye njia hiyo na ndie aliekuwa kwenye usukani
wakati meli hiyo Sewol ilipozama.
Kwa mujibu wa sheria Lee alikuwa
akitakiwa awe kwenye sitaha ya meli ambapo nahodha hutowa amri zake ili
kusaidiana na wenzake wakati meli ikipita kwenye maeneo ya bahari chafu.
Mwendesha mashtaka mwandamizi Yang
Jung-jin amewaambia waandishi wa habari nahodha huyo alikimbia kabla ya
abiria.Ukanda wa video uliorushwa na shirika la habari la Yonhap
umemuonyesha Lee akiwa miongoni mwa watu wa kwanza kuwasili ufukweni kwa
kutumia boti ya uokozi.
Yang amesema wafanyakazi hao wenzake
wawili waliokamatwa walishindwa kupunguza kasi ya mwendo wakati kivuko
hicho kikiwa karibu na visiwa na wameshindwa kuchukuwa hatua
zinazohitajika kuokowa maisha.
Kulikuwa na abiria 476 na mabaharia
kwenye meli hiyo ya tani 6,825 wakiwemo wanafunzi 320 na walimu 15
kutoka Shule ya Upili ya Danwon huko Ansan karibu na mji mkuu wa Seoul
wakati ilipoanza kupinduka na kuzama ikiwa safarini kutoka Incheon
kuelekea kisiwa cha kitalii cha Jeju kilioko kusini.
Afisa wa ulinzi wa mwambao Ko Myung-seok
amesema meli 176 na ndege 28 leo zimewekwa kufanya msako kwenye eneo
karibu na ilikozama meli hiyo na kwamba zaidi ya wapiga mbizi 650
wanajaribu kulifikia eneo la ndani ya meli hiyo iliozama Jumatano.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni