Stori: GLADNESS MALLYA NA CHANDE ABDALLAH
BOOOM! Katika hali ya kushangaza, mastaa
wawili Bongo, mwigizaji Wema Isaac Sepetu na mtangazaji wa DTV, Penniel
Mungilwa ‘Penny’ wanadaiwa kuipasua familia ya kinara wa Bongo Fleva,
Nasib Abdul ‘Diamond Platnumz’, Ijumaa Wikienda lina ripoti kamili.
Kwa mujibu wa chanzo makini ambacho ni
mtu wa karibu na familia hiyo kuna mgawanyiko ambao umesababisha mpasuko
unaofanya familia hiyo kuwa na makundi mawili yasiyoelewana juu ya
uhusiano wa Diamond na warembo hao.
Kwa sasa Diamond anatoka kimapenzi na
Wema baada ya kumwagana na Penny lakini mtangazaji huyo anadaiwa
kuendelea kwenda katika familia hiyo kwani asilimia kubwa inaonesha
anakubalika zaidi ya wengine wote.
TEAM PENNY VS TEAM WEMA
Habari zilidai kuwa mpasuko huo ni
mkubwa kwani kundi moja linalojiita Team Penny linamkubali zaidi Penny
na lingine ambalo lina watu wachache Team Wema linamkubali Wema.
Imefahamika kwamba kundi linalomkubali Penny na kumuona ndiye mwanamke
sahihi kuwa na Diamond japokuwa wameshaachana ni Mama Diamond mwenyewe,
Sanura Kassim ‘Sandra’, dada zake Esma Platnumz, Queen Darleen, Anko na
dada wa hiyari wa Diamond, Halima Haroun ‘Kimwana’
Ilidaiwa kwamba kundi hilo limekuwa
likitoa ushirikiano wa karibu mno kwa Penny na sehemu nyingi wanakuwa
wote ikiwemo kwenye sherehe na viwanja vya starehe, yaani ni fulu
kujiachia.
Habari hizo zilidadavua kuwa hata dada wa Diamond, Esma anaishi nyumba moja na wifi yake huyo wa zamani.
“Familia ya Diamond imegawanyika katika
makundi mawili, kundi kubwa linamkubali sana Penny japokuwa alishaachana
na Diamond. Ilisemekana kuwa si familia tu kwani hata madansa wa
Diamond wanampenda sana Penny kuliko Wema,” kilisema chanzo.
TEAM WEMA HII HAPA
Uchunguzi wa wanahabari wetu ulibaini
kuwa ndani ya kundi linalomtaka Wema kuna watu wachache akiwemo Diamond
mwenyewe, baba yake, Abdul Jumaa ambaye kwa upande wake alitamka wazi:
“Wema ndiye mkwe wa ukweli kabisa.”
Baba huyo alikwenda mbali na kusema
anamkubali Wema kwa sababu ana nyota kali na ana roho nzuri hivyo
akiendelea kuwa na mwanaye atakuwa na mafanikio tofauti na alivyokuwa na
Penny.
Pia ilijulikana kuwa kundi hilo lina mtu
mwingine, ndugu wa Diamond aitwaye Rommy Jones ambaye amekuwa
akionekana na Wema mara kwa mara hasa wakati msanii huyo akiwa
amesafiri.
HALIMA KIMWANA AITWA KIGEUGEU
Taarifa nyingine zilidai kwamba katika
sakata hilo, Halima kimwana amekuwa akiitwa kigeugeu kutokana na
kutokuwa na upande anaosimamia. “Mara utamuona na Wema ghafla unamuona
tena na Penny, yule hata haeleweki. Anajichetua sana,” kilisema chanzo
chetu.
MAMA DIAMOND ANASEMAJE?
“Mimi siwezi kumchagulia Diamond
mwanamke wa kuwa naye, yeye mwenyewe ataamua kwa sababu ni mtu mzima kwa
hiyo siwezi kumpangia au kumchagulia mwanamke wa kuwa naye,” alisema
mama Diamond bila kukanusha kuwa na ukaribu zaidi na Penny.
MSIKIE HALIMA KIMWANA
Baada ya kuwatafuta Diamond, Wema na
Penny bila mafanikio, Ijumaa Wikienda lilizungumza na Halima Kimwana
ambaye alikuwa na haya ya kusema:
“Sisi tuko karibu na Penny kwa sababu
anapenda kujichanganya na sisi hivyo hata Wema akija kutuchukua na
kutaka twende naye klabu hatukatai kwa sababu wote ni mawifi zetu.
“Hatubagui kwani hakuna siku ambayo Wema alishataka kuwa na sisi tukamkatalia.”
MASWALI
Hivi karibuni picha za Penny akiwa na
mawifi zake kwenye shughuli ya kumtoa mtoto wa ndugu yao zilivuja ambapo
ndani ya sherehe hiyo pia Diamond alikuwepo akiwa anacheza dufu lakini
Wema hakuonekana, jambo lililozua maswali.
GPL
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni