Mrembo
huyo alikamatwa Desemba 19, mwaka jana katika Uwanja wa Ndege wa Macau
akitokea Bangkok, Thailand akiwa na kete 57 (kilo 1.1) za unga aina ya
heroin tumboni zikiwa na thamani ya shilingi milioni 300.
TAARIFA MBICHI
Taarifa
mbichi kabisa zinadai kwamba, Jack amepewa mwaka mmoja na nusu (siku
447) ajifunze lugha inayozungumzwa na watu wa Macau (Kireno) ambayo
ndiyo itakayotumika mahakamani wakati kesi yake itakapoanza kuunguruma.
Dawa za kulevya alizokutwa nazo Jack Patrick.
Sheria
ya kisiwa hicho inasema kuwa mshitakiwa yeyote atakayefikishwa kortini,
kesi yake haitasikilizwa mpaka majaji wakubali kwamba anajua lugha hiyo
na si kinyume na hapo.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, mwalimu maalum anayejua Lugha za Kiingereza na Kireno ndiye atakayemfundisha Jack mpaka atakapojua.
AKIJUA MAPEMA ITAMSAIDIA
Habari za ndani kutoka vyanzo
vya uhakika nchini humo zinasema kwamba, kama Jack angekuwa anakijua
Kireno angepandishwa kizimbani mara baada ya upelelezi kukamilika, Machi
mwaka huu.
KIFUNGO CHA CHINI MIAKA 16
Habari nyingine mpya kutoka
Macau zinasema kuwa, sheria za eneo hilo kuhusu makosa ya kukutwa na
madawa ya kulevya, mtuhumiwa akitiwa hatiani kifungo cha chini ni miaka
16 kulingana na mwenendo wa kesi.
SERIKALI YA TANZANIA YASUBIRI ORODHA…
Juzi, Uwazi liliwasiliana kwa
simu ya mkononi na Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa
ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa na kumuuliza kuhusu nini kinaendelea
kati ya serikali na utawala wa Macau kufuatia Mtanzania, Jack Patrick
kunaswa na unga nchini humo.
Nzowa: “Aaah! Sisi tumetuma
maswali yetu kule (Macau) kupitia Polisi wa Kimataifa (Interpol),
tumetaka kujua kama huyo binti (Jack) amewataja vigogo waliomtuma ni
majina gani wanayo.
“Ndiyo tunasubiri majibu yao
ili tujue nini kinaendelea kule. Kama aliwataja watu tutaanza
kuwafuatilia mara moja maana lazima kuna vigogo nyuma yake.”
KWA NINI MABOSI WA KUBEBA UNGA HUWA HAWATAJWI?
Kinachomshangaza Kamanda Nzowa ni usiri wa watu wanaodaiwa kukamatwa na unga kufunga vinywa vyao kuwataja vigogo waliowatuma.
Inadaiwa moja ya kiapo kikubwa
kabla mtu hajaanza kuwa ‘punda’ (kubebeshwa madawa ya kulevya) ni
kusema ‘piga, ua, galagaza’ katu hawezi kutaja wahusika wenye mzigo.
“Unajua kwa sababu gani? Wale
wanaobeba wanaambiwa mkikamatwa msitutaje hata iweje ili tufanye mipango
ya kuwatoa. Sasa mtu anaona nikitaja sintatoka, ndiyo anaamua kuendelea
kuishi na siri yake halafu na wao wakubwa wao wanakuwa hawana habari
nao,” alisema Nzowa.
KUMBE JACK ALIPEWA MAJI YA MOTO
Habari zaidi zinasema kuwa,
siku ya tukio la kukamatwa, Jack alikataa kwamba hajabeba kete za unga
tumboni, askari wa uwanjani wakampa maji ya moto ili anywe.
“Kwa mtu aliye na kete
tumboni, hawezi kukubali kunywa maji ya moto kwani huyeyusha kete
zilizomo ndani na kuweza kusababisha kifo chake.
“Jack alikataa kunywa maji ya
moto, hilo likachangia askari kuamini ana kete tumboni, ndiyo maana
walimpeleka chooni kuzitoa kitaalam,” kilisema chanzo.
RAY C AWASHANGAZA WENGI
Kufuatia sakata la Jack, hivi
karibuni, staa wa muziki wa kizazi kipya Tanzania, Rehema Chalamila ‘Ray
C’ aliingiza kwenye mtandao wake wa kijamii akitoa maoni kwamba Jack
apewe adhabu kali zaidi ya kifungo (pengine kunyongwa) hali
iliyowashangaza wengi waliotembelea mtandao huo.
Baadhi ya watu waliozungumza na Uwazi baada ya staa huyo kuingiza mawazo yake walimshutumu wakisema alitakiwa kutafakari upya.
“Yule dada (Ray C) hakutakiwa
kumtakia mwenzake mabaya zaidi, kama yeye aliathirika na madawa na
amepona anatakiwa kuwa balozi kwa wengine na si kuwahukumu wenzake,”
alisema Joan Mushi, mkazi wa Sinza ‘E’ jijini Dar.
WAZIRI MEMBE VIPI?
Juzi, Uwazi lilimtafuta Waziri
wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Kamillius
Membe ili azungumze lolote kuhusu sakata la Jack Patrick lakini
hakupatikana badala yake naibu wake, Mahadhi Maalim alisema taarifa za
Jack kukamatwa amezisikia kupitia vyombo vya habari na hana habari
kiundani ila bosi wake anaweza kuwa na maelezo zaidi.
WOLPER, AUNT EZEKIEL, WEMA, WANAWINDWA KUWA ‘MAPUNDA’
Wakati Jack akiwa katika
mazito hayo, habari ambazo zilifika kwenye dawati la Uwazi dakika za
mwisho zinasema mastaa wa filamu za Bongo, Jacqueline Massawe Wolper,
Aunt Ezekiel Grayson na Wema Isaac Sepetu wamekuwa wakitolewa udenda na
vigogo wa unga.
Vigogo hao wamekuwa wakihaha
kutafuta namna ya kuwaingiza mastaa hao kwenye ‘chaneli’ yao ili wawe
mapunda wa kubeba kete za unga kupeleka ughaibuni wakiamini kuwa, mastaa
hawakamatwi hovyo uwanja wa ndege, hususan wa Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni